Mar 09, 2016 15:24 UTC
  • Ayatullah Makarim Shirazi: Viongozi wa Kiarabu hawawezi kuficha mafanikio ya kujivunia ya Hizbullah

Ayatullah Nassir Makarim Shirazi mmoja wa Marajii Taqlidi wa nchini Iran amesema kuwa, viongozi wa Kiarabu katu hawawezi kuficha mafanikio ya kujivunia ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon.

Kiongozi huyo wa kidini mwenye makao yake mjini Qum hapa Iran amebainisha kwamba, hatua ya viongozi wa Kiarabu ya kupasisha maazimio ya aibu dhidi ya Hizbullah katu haiwezi kuficha mafanikio ya kujivunia ya harakati hiyo ya mapambano, kwani Hizbullah itaendelea kubakia kuwa ni shujaa na bingwa.

Ayatullah Makarim Shirazi ameongeza kwamba, historia ya Waarabu imeshuhudia mara chache sana ushujaa na ujasiri kama wa Hizbullah ya Lebanon kwani harakati hiyo imeweza kuushinda utawala ghasibu wa Israel uliokuwa haushindwi.

Ikumbukwe kuwa, Jumatano iliyopita Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi liliiweka harakati ya Hizbullah ya Lebanon katika orodha ya makundi ya kigaidi na kutangaza kuwa, limechukua hatua kadhaa katika uwanja huo. Hatua ya baraza hilo linaloundwa na nchi za Saudi Arabia, Qatar, Kuwait, Oman, Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain imekabiliwa na upinzani mkubwa ndani na nje ya Lebanon. Asasi na harakati mbalimbali za kieneo na kimataifa zimelaani vikali hatua hiyo ya Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi.